Catholic Daily Prayers.

About

Welcome to the Digital Sanctuary

May peace be with you as you pray today.

Verse of the Day

† Kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Amina

Baba yetu uliye mbinguni, jina lako litukuzwe, ufalme wako ufike, utakalo lifanyike dunian kama huko mbinguni, utupe leo mkate wetu wa kila siku, utusamehe makosa yetu kama nasi tunavyowasamehe wale waliotukosea usitutie katika vishawishi lakini utuopoe maovuni. Amina

Salamu Maria, umejaa neema Bwana yu nawe, umebarikiwa kuliko wanawake wote na uzao wa tumbo lako amebarikiwa, Maria mtakatifu Mama wa Mungu utuombee sisi wakosefu kama tunavowasamehe na sisi waliotukosea usitutie katika vishawishi lakini utuopoe maovuni. Amina.

Atukuzwe baba na mwana na roho mtakatifu kama mwanzo na sasa na Siku zote na milele Amina

"Malaika wa Bwana alimpasha habari Maria. Naye akapata mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu. Salamu, Maria..... Ndimi mtumishi wa Bwana. Nitendewe ulivyonena. Salamu, Maria.... Neno la Mungu akatwaa mwili. Akakaa kwetu. Salamu, Maria.... Utuombee, Mzazi mtakatifu wa Mungu. Tujaliwe ahadi za Kristu. Tuombe Tunakuomba, Ee Bwana, utie neema yako mioyon mwetu, ili sisi tuliojua kwa maelezo ya Malaika kwamba Mwanao amejifanya mtu kwa mateso na msalaba wake tufikishwe kwenye utukufu na ufufuko. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu Bwana wetu. Amina"

Malkia wa mbingu, furahi Aleluya, Kwani uliyestahili kumchukua Aleluya, Amefufuka alivyosema Aleluya Utuombee kwa Mungu Aleluya Furahi, shangilia, Ee Bikira Maria Aleluya, Kwani hakika Bwana amefufuka Aleluya. Tuombe: Ee Mungu uliyependa kuifurahisha dunia kwa kufufuka kwake Bwana wetu Yesu Kristu, Mwanao; fanyiza twakuomba, kwa ajili ya Bikira Maria, tupate nasi furaha za uzima wa milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu Bwana wetu. Amina.

Nasadiki kwa Mungu, Baba Mwenyezi, muumba mbingu na dunia. Na kwa Yesu Kristu, Mwanaye wa pekee, Bwana wetu; aliyetungwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, akazaliwa na Bikira Maria, akateswa kwa mamlaka ya Ponsyo Pilato, akasulubiwa, akafa, akazikwa, akashukia kuzimu; siku ya tatu akafufuka katika wafu; akapaa mbinguni; amekaa kuume kwa Mungu Baba Mwenyezi; toka huko atakuja kuwahukumu wazima na wafu. Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Kanisa takatifu katoliki, ushirika wa Watakatifu, maondoleo ya dhambi, ufufuko wa miili na uzima wa milele. Amina.

Mungu wangu, nasadiki maneno yote linalosadiki na linalofundisha kanisa katoliki la Roma; Kwani ndiwe uliyefundisha hayo, wala hudanganyiki, wala hudanganyi. Amina

Mungu wangu, natumaini kwako nitapewa kwa njia ya Yesu Kristu, neema zako duniani na utukufu mbinguni, kwani ndiwe uliyeagana hayo nasi, nawe mwamini. Amina

Mungu wangu, nakupenda zaidi ya cho chote, kwani ndiwe mwema, ndiwe mwenye kupendeza. Nampenda na jirani yangu kama nafsi yangu, kwa ajili yako. Amina

"Na tuwaze katika moyo makosa yote ya leo tuliyomkosea Mungu, Namuungamia Mungu Mwenyezi, nanyi ndugu zangu, kwani nimekosa mno, kwa mawazo, kwa maneno, kwa vitendo na kwa kutokutimiza wajibu, nimekosa mimi, nimekosa mimi, nimekosa sana. Ndio maana nakuomba Maria mwenyeheri, Bikira daima, Malaika na Watakatifu wote, nanyi ndugu zangu, niombeeni kwa Bwana Mungu wetu. +Mungu Mwenyezi atuhurumie, atusamehe dhambi zetu na atufukishe kwenye uzima wa milele, Amina. SALA YA KUTUBU. Mungu wangu, nimetubu sana niliyokosa kwako. Kwani ndiwe mwema, ndiwe mwenye kupendeza. Wachukizwa na dhambi, basi sitaki kukosa tena. Nitafanya kitubio, naomba neema yako nipate kurudi. Amina. Ee Mungu mwenye huruma, uwashushie baraka zako, Baba Mtakatifu wetu {Jina la Papa} na maaskofu, na mapadre, na mashemasi, wakulima, wafanyakazi wote, wanafunzi na jamii yote unaowafanya kuwa watu wako . Uwaokoe washenzi, uwafariji wagonjwa, waelekee wanaozimia waweze kuona mwanga wa milele, Amina.

Malaika mlinzi wangu, unilinde katika hatari zote, za roho na za mwili. Amina. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu. Kama mwanzo na sasa na siku zote na milele. Amina

Tubariki Mungu wetu, sisi na chakula chetu tupate nguvu za kukutumikia vyema. Amina.

Nakushukuru Mungu wangu, mimi na chakula ulichonijalia, nipate nguvu za kukutumikia vema. Amina.

† Kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Amina

Ee Yosefu mwenye heri, tunakimbilia kwako katika masumbuko yetu; na kisha omba shime ya mchumba wako mtakatifu tunaomba pia kwa matumaini usimamizi wako. Kwa ajili ya mapendo uliyompenda Bikira Mtakatifu mzazi wa Mungu, na kwa ajili ya kumtunza mtoto Yesu, twakuomba sana, utuangalie kwa wema siye tuliokuwa fungu lake Yesu Kristu, tukakombolewa kwa damu yake. Tusimamie katika masumbuko yetu kwa enzi na shime yako. Ee mlinzi amini wa jamaa takatifu, uwakinge watoto wateule wa Yesu Kristu. Ee Baba uliyetupemda mno tuepushe na kilema chochote cha madanganyo na upotevu. Ee kinga yetu mwezaji, utusimamie huko juu Mbinguni ulipo, tunaposhindana na wenye nguvu wakaao gizani. Kama vile siku za kale ukamwopoa mtoto Yesu katika hatari ya kuuawa na leo hivi likinge Kanisa Takatifu la Mungu katika mitego ya adui, na katika shida zote. Mtunze daima kila mmoja wetu kwa mfano wako, ili tupate na msaada wako, kukaa na utakatifu maisha, kufa kifo chema, na kupata Mbinguni makao ya raha Milele. Amina.

Mtakatifu Mikaeli Malaika Mkuu, utulinde katika vita, uwe kinga yetu katika maovu na maoteo ya shetani, Mungu amtiishe tunaomba sana, nawe Mkuu wa Majeshi ya Mbinguni, kwa nguvu ya Mungu, uwaangushe motoni shetani na pepo wabaya wengine wote, wanaozunguka duniani, ili kuzipoteza roho za watu. AMINA.

Ee Bwana unifanye kuwa chombo cha amani yako. Palipo chuki unifanye nieneze mapendo. Palipo na mashaka pawe na amani. Palipo na tuamini pawe na matumaini. Palipo na giza pawe na mwanga. Palipo na huzuni pawe na furaha. Ee Bwana Mungu,unijalie nisitafute kufarijiwa,bali kufariji, kupendwa bali kupenda, kwani ni kwa kutoa ndipo tunapokea, ni kwa kusamehe ndipo tunasamehewa na ni kwa kufa ndipo tunapokea uzima wa Milele. AMINA.

Ee Mtakatifu Antoni wa Padua, uliye mpole kati ya watakatifu wote.Upendo wako kwa Mungu na kwa binadamu wakati ulipoishi hapa duniani, umetustahilia uwezo wa kutenda miujiza mingi kwa ajili ya wale wenye shida. Kwa hiyo sisi pia tunapata moyo wa kukimbilia kwako na kuomba msaada wako. Labda ombi letu haliwezi kutimizwa bila mwujiza. Hata hivyo huitwi Mtakatifu wa miujiza? Kwa hiyo Mtakatifu Antoni wa Padua mwenye upole na huruma sana kwa watu wenye shida, sikiliza maombi yetu na kuyapeleka mbele ya Mtoto Yesu aliyependa kukaa mikononi mwako.Nasi tutakuonyesha shukrani kubwa katika maisha yetu yote. Amina.

Ee Yesu, uliyejaa neema na upendo, ukijitoa sadaka kwetu, hata kufa msalabani. Nakusihi kwa unyenyekevu unijalie neema zako kwa maombezi ya mtumishi wako, Mt. Pio wa Pietrelcina. Alishiriki kwa ukarimu mateso yako, akakupenda sana na kufanya kazi kwa uaminifu kabisa kwa ajili ya utukufu wa Baba yako wa Mbinguni na kwa ajili ya wokovu wa watu. Kwa hiyo nakusihi kwa matumaini, unijalie kwa maombezi yake, neema ya {....} ambayo naihitaji Sana. Atukuzwe Baba...(Mara 3).

Mtakatifu Agatha, Bikira aliyebarikiwa na Mungu. Unaheshimiwa kama mlinzi wa Saratani ya matiti. Ulipata maumivu na kuteswa katika kujitolea kwako kwa Bwana. Nilinde kutokana na Saratani ya matiti na kuingilia kati mbele ya Mungu Mwenyezi, Na niombee ili nipate kuponywa. Niponye na unifariji na kwa rehema, Nipe ulinzi kutoka kwa saratani yote. Mtakatifu Agatha, uniombee. AMINA.

Ee Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu, ulistahili kuitwa Msimamizi wa Misioni Katoliki za dunia yote. Kumbuka ile tamaa yako kuu uliyoonyesha huku duniani ya kusimika Msalaba wa Yesu Kristu, katika nchi zote, na kuhubiri Injili mpaka mwisho wa dunia. Twakuomba kwa ajili ya maagano yako, wasaidie mapadre,wamisionari, na Kanisa zima. Ee Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu "Msimamizi wa misioni"--- Utuombee.Amina

Ee Mtakatifu Yuda,mtume na shahidi,uliye mkuu katika fadhila natajiri wa miujiza,jamaa wa karibu wa Yesu Kristo,mwombezi mwaminifu wa wale wote waombao msaada wako nyakati za shida.Ninakukimbilia wewe na kukusihi unisaidie,wewe uliyepewa uwezo mkubwa na Mungu. Unisaidie katika shida yangu hii....(Taja ombi lako). Nami ninaahidi kukufanya ili ujulikane na watu wakuombe. Sali
· Baba yetu tatu, x3
· Saalamu Maria x3
· Atukuzwe x3
Mtakatifu Yuda,utuombee wote tuombao msaada wako. AMINA

Mtukufu Mt.Anna,uliyejawa huruma kwa waote wakuombao,na upendo kwa wale watesekao,nikielemewa na uzito wa matatizo yangu,ninajitupa miguuni pako na kukuomba unisaidie haja yangu ninayoileta kwako chini ya ukingaji wako wa pekee. Upende kuifikisha kwa binti yako Bikira Maria na kuiweka mbele ya kiti cha enzi cha Yesu,ili apate kuikubali.Usiache kuniombea hadi ombi langu litakapokubaliwa.Juu ya yote unipatie neema ya kumtazama siku moja Mungu uso kwa uso,nami pamoja nawe na Maria na watakatifu wote tumsifu na kumtukuza kwa milele yote. Ee mwema Mt. Ana, mama wa yule aliye uzima,tulizo na matumaini yetu,utuombee na kutupatia ombi letu.(x3)

† Kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Amina

Ee Bwana Yesu Kristo, ulishiriki ubinadamu wetu kwa hiari yako upate kuwaponya wagonjwa na kuwaokoa wanadamu. Sikiliza kwa huruma sala zetu, umjalie afya ya mwili na roho (Taja jina la mgonjwa) yetu.Mfariji kwa kinga yako, mpe nafuu kwa nguvu yako. Msaidie atumaini kuokoka kwa njia ya mateso, kama ulivyotufundisha kutumaini hapo ulipoteswa kwa ajili yako. Utujalie sisi sote amani na furaha zote za ufalme wako huko unakoishi daima na milele.Amina

Ee Mungu wa milele usiyezeeka, uliyeumba kila kitu kwa utaratibu, Wewe ambaye ni chanzo cha ufahamu na busara yetu, unayeangaza akili zetu kwa mwanga wa imani. Tia ndani ya akili yangu tone la busara na maarifa yako; ondoa giza la kutofahamu kwangu. Unipe uwezo wa kuongea kwa ufasaha; uweke maneno yako mdomoni mwangu, unijalie uwezo wa kuandika na kufikiri kwa hekima, unijalie kipawa cha kukumbuka yote ninayojifunza na kipawa cha kufafanua sawasawa yote ninayosoma. Nawe Mama yangu imakulata, kikao cha hekima ya Mungu, uwe Mwombezi wangu kwa mwanao Yesu Kristo. Ee mpendwa Mtakatifu Rita, uniombee ili nipate zaidi ya yote mwanzo wa hekima ambayo ni kumcha Mungu, na toka hapo niwe Mkristo mwema. Ninaomba hayo yote kwa njia ya Kristo Bwana wetu aliye hekima na ufahamu wa milele, AMINA.

Ee Mt. Yosefu,Mtukufu mfano wa wafanyakazi wote, uniombee nipate neema ya kufanya kazi katika roho ya toba kwa ajili ya kufidia dhambi zangu nyingi, ili nifanye kazi kwa uaminifu nikithamini zaidi hisia ya wajibu kuliko upendeleo binafsi, ili nifanye kazi kwa furaha na shukrani nikihesabu kuwa ni fahari uwezo wa kuvitumia na kuvikuza kwa njia ya kazi vipaji nilivyopata kutoka kwa Mungu. Nifanye kazi kwa utaratibu, amani, kiasi na uvumilivu kutokubali kushindwa na uchovu na matatizo, ili zaidi ya yote nifanye kazi kwa nia safi na kujisahau mwenyewe nikikumbuka wakati wote juu ya kifo na bili ambayo itanibidi niilipe kwa ajili ya muda niliopoteza, vipaji nisivyotumia, kupuuza nafasi ya kutenda mema na upendeleo mtupu wa mafanikio wenye kuleta madhara katika kazi ya Mungu. Yote kwa ajili ya Yesu, yote kwa njia ya Maria, Yote kwa mfano wako, Ee Baba Mt. Yosefu. Huu uwe wito wangu katika maisha na saa ya kufa kwangu. Amina.

Mungu wetu uliyetoa amri tuwapende, tuwaheshimu, tuwatii na kuwasaidia Wazazi na Walezi wetu, usikilize Sala tunazokutolea, kwa kuombea Wazazi na Walezi wetu, wanatufanyia mema mengi hata hatuwezi kabisa kuwalipa sawa. Tangu Utoto wetu wanatulinda, wanatutunza wanatupatia Chakula na Mavazi, wanatuangalia Mchana na Usiku. Wanachoka wanakosa usingizi wapate kutulinda na kututuliza, wanahangaika sana na hata kupata uchungu kwa ajili yetu. Ee Mungu, uwarudishie mema yote wanayotufanyia uwabariki na kuwalinda Roho na Mwili. Uwasaidie katika kazi zao zipate kuwafaa sana. Uwatulize uchungu wa roho wapate kufurahiwa siku zote. Uwakinge na hatari zote za Roho na za Mwili. Uwalinde waone uzee mzima na mwema, wakafurahiwe na kuona mwenendo mwema wa Watoto wao. Utusaidie nasi tuwapende sana, tuwatil siku zote, tuwafurahishe mioyo yao kwa kuwatunza na kuwaheshimu. Uwalinde siku zote za Uzee wao, wakidumu katika urafiki nawe, hatimae ukatupokee wote, pamoja Mbinguni, tupate kupendana na kufurahi katika Utukufu wako Milele. Amina.

Ee Mungu, ambaye ulipoumba binadamu uliweka kwamba mume na mke wawe mmoja, tunaomba uwabariki, katika kiungo cha upendo usiotengana, wale waliounganishwa katika agano la Ndoa, ili, kama unavyozaa matunda ya upendo wao, wawe, kwa neema yako, mashahidi wa upendo wenyewe. Kupitia Kristo Bwana wetu. Amina.

Mungu Baba yetu, umetubariki sisi kwa zawadi ya Watoto, tunakushukuru kwa Lulu hizi za thamani zinazopamba nyumba yetu, kicheko chao kinatupatia sisi furaha na kuyang’arisha Maisha yetu, wenyewe ni Mwelezo wa uwepo wako katika nyumba yetu, kukua kwao kunaonyesha mafumbo ya upendo wako, wawezeshe kuonja uwepo wa upendo wako na kukomaa jatika Hekima na kukua katika upendo wako, Maisha yajayo ya Watoto wetu yapo mikononi mwako, japokuwa nasi tuna jukumu katika kuelekeza mwelekeo wao wa baadae, Tusaidie kuwa waaminifu katika jukumu ketu ili kwamba tuweze kuwasaidia katika kuitikia Neema zako na hivyo wawe kama vile unavyotaka wawe. Amina. #TuwaleenaTuwalindeWatoto #SalaniSilaha #RadioMariaTz

Ee mwumba wetu, umewaunganisha watu katika ndoa Takatifu, nami natumaini kupokea Sakramenti hiyo na kushirikiana na mwenzangu wa ndoa maisha yangu yote. Kwa hiyo nakuomba Ee Bwana unisaidie kuchagua kwa hekima, nipate mchumba mwema, safi na mwaminifu, nifuate zaidi uzuri wa roho kuliko wa uso, zaidi tabia njema kuliko umaridadi. Mioyo yetu iwe ya kulingana na nia zetu zipatane, tupate kuishi pamoja na amani na kulea jamaa zetu kwa kukuheshimu wewe na baraka zako. Amina.

† Kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Amina

1. Kanuni ya Imani... 2. Baba Yetu... 3. Ee Bwana Utujalie Imani--- Salamu Maria... 4. Ee Bwana Utujalie Matumaini--- Salamu Maria... 5. Ee Bwana Utujalie Mapendo--- Salamu Maria... Inafwata Matendo ya Rozari hapo chini....

Kumbuka ee Bikira mwenye rehema,haijasikika kamwe kwamba ulimwacha mtu aliyekimbilia ulinzi wako, akiomba msaada wako,akitaka umwombe.Nami kwa matumaini hayo nakukimbilia ee mama,mkuu wa mabikira,ninakuja kwako,ninasimama mbele yako,nikilalamika mimi mkosefu ewe mama wa neno la Mungu,usiyakatae maneno yangu,mbali uyasikilize kwa wema na unitimizie Amina.

Bwana utuhurumie. Bwana utuhurumie. Kristo utuhurumie. Kristo utuhurumie. Bwana utuhurumie. Bwana utuhurumie. Kristo utusikie. Kristo utusikilize Baba wa mbinguni, Mungu, utuhurumie. Mwana Mkombozi wa dunia, Mungu, utuhurumie. Roho Mtakatifu, Mungu, utuhurumie. Utatu Mtakatifu, Mungu mmoja, utuhurumie. KIITIKIO: Utuombee Maria Mtakatifu, Mzazi Mtakatifu wa Mungu, Bikira Mtakatifu, Mkuu wa mabikira, Mama wa Kristu, Mama wa neema ya Mungu, Mama mtakatifu sana, Mama mwenye usafi wa moyo, Mama usiye na doa, Mama usiye na dhambi, Mama mpendelevu, Mama mstaajabivu, Mama wa shauri jema, Mama wa Mwumba, Mama wa Mkombozi, Bikira mwenye utaratibu, Bikira mwenye heshima, Bikira mwenye sifa, Bikira mwenye enzi, Bikira mwenye huruma, Bikira amini, Kikao cha haki, Kikao cha hekima, Sababu ya furaha yetu, Chombo cha neema, Chombo cha heshima, Chombo bora cha ibada, Waridi lenye fumbo, Mnara wa Daudi, Mnara wa pembe, Nyumba ya dhahabu, Sanduku la Agano, Mlango wa mbingu, Nyota ya asubuhi, Afya ya wagonjwa, Makimbilio ya wakosefu, Mfariji wa wenye uchungu, Msaada wa Wakristu, Malkia wa Malaika, Malkia wa Mababu, Malkia wa Manabii, Malkia wa Mitume, Malkia wa Mashaidi, Malkia wa Waungama, Malkia wa Mabikira, Malkia wa Watakatifu wote, Malkia uliyeumbwa, pasipo dhambi ya asili, Malkia uliyepalizwa mbinguni, Malkia wa Rozari takatifu, Malkia wa amani. Mwanakondoo wa Mungu uondoaye dhambi za ulimwengu, utusamehe, Bwana. Mwanakondoo wa Mungu uondoaye dhambi za Ulimwengu, utusikilize, Bwana. Mwanakondoo wa Mungu uondoaye dhambi za ulimwengu, utuhurumie. K. Utuombee, Mzazi Mtakatifu wa Mungu. W. Tujaliwe ahadi za Kristu. TUOMBE: Ee Bwana Mungu, utujalie sisi watumishi wako afya ya roho na ya mwili sikuzote. Tuopolewe na mashaka ya sasa kwa maombezi ya Maria mtakatifu, Bikira daima, ili tupate na furaha ya milele. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristu Bwana wetu. Amina.

† Kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Amina

1. Baba Yetu... 2. Ee Bwana Utujalie Imani--- Salamu Maria... 3. Ee Bwana Utujalie Matumaini--- Salamu Maria... 4. Ee Bwana Utujalie Mapendo--- Salamu Maria... 5. Kanuni ya Imani... Zinafwata Punje za Rozari hapo chini....

Kwenye Punje Kubwa (badala ya Baba Yetu): Baba wa Milele, ninakutolea Mwili na Damu, Roho na Umungu, wa Mwanao Mpenzi sana Bwana wetu Yesu Kristo, kwa malipizi ya dhambi zetu, na dhambi za dunia nzima. + Kila penye punje ndogo (badala ya Salamu Maria): Kwa ajili ya mateso makali ya Bwana Wetu Yesu Kristo... Utuhurumie sisi na dunia nzima. Mwisho wa Rozari sali mara tatu (3)sala ifuatayo : Mungu Mtakatifu, Mtakatifu mwenye Enzi, Mtakatifu Usiyeweza kufa, Utuhurumie sisi na dunia nzima.

Bwana utuhurumie – Bwana utuhurumie. Kristu utuhurumie – Kristu utuhurumie. Bwana utuhurumie – Bwana utuhurumie. Kristu utusikie – Kristu utusikilize. Baba wa mbinguni Mungu – utuhurumie Mwana Mkombozi wa dunia Mungu – utuhurumie Roho Mtakatifu Mungu – utuhurumie Utatu Mtakatifu Mungu mmoja –utuhurumie. Huruma ya Mungu iliyo sifa kuu ya Muumba wetu ~Tunakutumainia [KIITIKIO: Tunakutumainia] Huruma ya Mungu iliyo kilele cha ukamilifu wa Mwokozi wetu. Huruma ya Mungu iliyo upendo usiopimika wa Roho Mtakasa. Huruma ya Mungu fumbo lisilofahamika la Utatu Mtakatifu Huruma ya Mungu iliyo ishara ya uwezo mkuu wa Mungu Mwenyezi. Huruma ya Mungu iliyofumbuliwa katika kuziumba Roho za Malaika wa mbinguni. Huruma ya Mungu iliyotuumba na kutuamuru tuwepo bila kutokana na chochote. Huruma ya Mungu inayotujalia maisha ya kutokufa. Huruma ya Mungu inayotukinga na adhabu tunazostahili. Huruma ya Mungu inayotuinua tutoke katika taabu, unyonge na maumivu ya dhambi zetu. Huruma ya Mungu inayotufanya wenye haki katika Neno aliyejifanya Mtu. Huruma ya Mungu inayofurika kutoka katika majeraha ya Kristu. Huruma ya Mungu inayobubujika kutoka ndani ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Huruma ya Mungu iliyotupatia Bikira Maria Mtukufu awe kwetu Mama wa Huruma. Huruma ya Mungu iliyoonyeshwa katika kuanzishwa Kanisa Katoliki. Huruma ya Mungu inayopatikana katika mafumbo ya Sakramenti Takatifu. Huruma ya Mungu inayotolewa kwa wanadamu wote kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo na Kitubio. Huruma ya Mungu inayotolewa katika Sakramenti ya Ekaristi na Upadrisho. Huruma ya Mungu inayoonyeshwa kwetu pale inapotuita na kutuingiza katika kuwatakatifuza wenye haki. Huruma ya Mungu inayotimilika katika ukamilifu wa watu watakatifu. Huruma ya Mungu chemchemi ya afya kwa wagonjwa na wote wanaoteseka. Huruma ya Mungu iliyo faraja ya wote wenye uchungu moyoni. Huruma ya Mungu iliyo tumaini la roho zinazosumbuliwa na mkato wa tamaa. Huruma ya Mungu iliyo mwenzi wa daima na popote wa watu wote. Huruma ya Mungu inayowahi kutuletea neema zake. Huruma ya Mungu iliyo amani yao wanaokufa. Huruma ya Mungu iliyo burudisho na faraja yao marehemu wa toharani. Huruma ya Mungu iliyo furaha ya mbinguni kwa watakatifu wote. Huruma ya Mungu iliyo taji la watakatifu wote. Huruma ya Mungu chemchemi ya miujiza isiyokauka. Mwanakondoo wa Mungu uliyetuonyesha huruma yako kuu katika kuikomboa dunia kwa msalaba wako mtakatifu, ~ Utusamehe Ee Bwana. Mwanakondoo wa Mungu unayejitolea kwetu kwa mapendo na huruma katika kila adhimisho la Sadaka ya Misa Takatifu, ~ Utusikilize Ee Bwana. Mwanakondoo wa Mungu anayeondoa dhambi za dunia kwa njia ya huruma yako isiyo na mwisho ~ Utuhurumie. Kiongozi: Bwana utuhurumie – Wote: Kristu utuhurumie, Bwana utuhurumie. Kiongozi: Huruma anana za Bwana zi juu ya kazi zake zote – Wote: Huruma za Bwana nitaziimba milele. Tuombe: Ee Mungu uliye na huruma isiyo na mwisho, na hazina za wema na upendo wako hazina mipaka. Tunakusihi ututazame sisi watu wako huku duniani na kutuongezea huruma yako tena na tena, ili itusaidie tusije tukakata tamaa hata mara moja, haidhuru tukumbane na majaribu makubwa kiasi gani, bali tuweze daima kuzielekea na kuzishika amri zako, kwa matumaini na kutimiza mapenzi yako matakatifu, ambayo ndiyo huruma yenyewe. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristu Mwanao, Mfalme wa Amani na Huruma, aishiye na kutawala nawe, na Roho Mtakatifu, kwa pamoja mkituonyesha huruma, daima na milele. Amina.